UMEWAHI KUWASIKIA VIDUKARI AU WADUDU MAFUTA? (Aphids)

Karibu katika makala zetu na leo hii tunakuletea undani hasa wa aphids maarufu kama wadudu mafuta au vidukari.

VIDUKARI/WADUDU MAFUTA

Hawa ni aina ya wadudu waharibifu wa mazao ambao hushambulia mimea karibu yote hususani mazao ya mboga mboga. Kisayansi wanajulikana kama Aphis gossypii na kwa Kiswahili ni maarufu kama vimamba, vidukari au wadudu mafuta.

Wadudu hawa wana hutofautiana kwa rangi na rangi kuu ambazo huwa nazo ni kijivu, nyeusi au kijani na huonekana kwenye maeneo ya chini ya majani. Huwezi kumkuta kidukari akiwa mmoja tu, mara zote huwa wanakuwa wengi kwa makundi na hivyo kuleta uharibifu mkubwa.

Wajue Aphids maarufu kama vidukari au wadudu mafuta

ATHARI ZA VIDUKARI

Vidukari hushambulia sana mazao wakati wa kiangazi na miongoni mwa athari wanazoleta katika mimea ni pamoja na:

  • Kufyonza maji ya kwenye majani
  • Kubadillisha umbo la majani na kuyafanya yajikunje
  • Hupunguza uwezo wa mmea kujitengenezea chakula na kufanya majani kuwa ya njano.
  • Athari hizi hupelekea mmea kukosa afya na hatimaye kufa.
  • Pia wanabeba virusi ambavyo wanaweza kuvisambaza kwa urahisi kutoka mmea mmoja kwenda mwingine.

JINSI YA KUDHIBITI VIDUKARI

Ni muhimu kuchukua hatua ya kuwadhibiti mapema kabla hawajaleta madhara makubwa. Endapo tahadhari isipochukuliwa madhara yanaweza kuwa makubwa kwani vimamba huzaliana kwa wingi na kwa haraka. Miongoni mwa njia za kuwadhibiti ni pamoja na:

  1. Panda wakati wa msimu. Kwa mazao ambayo yanaweza kulimwa wakati wa mvua, basi yalimwe wakati huo ili kupunguza uwezekano wa kushambuliwa na vidukari.
  2. Panda mazao yanayoweza kufukuza vidukari kama vile vitunguu swaumu (garlic) na vitunguu maji kuzunguka shamba; hii itakusaidia kupunguza uwezekano wa vidukari kuwepo lakini pia utavuna na zao jingine mbadala wa zao kuu ulilokusudia.
  3. Matumizi ya maadui wa asili kama ladybugs, lacewings; hawa wanaweza kununuliwa kwenye maduka ya pembejeo za kilimo hai au wanaweza kupatikana shambani kwa kupanda mazao ambayo yanaweza kuwavutia wadudu hawa. Mfano karafuu, mnanaa (mint) na binzari (dill).
  4. Mwagilia maji kwa msukumo mkubwa kwenye mazao. Njia hii ina changamoto kwani kwa mazao ambayo ni laini na ambayo hayana shina imara ni rahisi kuharibiwa na maji yenye msukumo mkubwa.
  5. Tumia mchanganyiko wa maji na sabuni. Changanya maji na sabuni na upulizie mchanganyiko huo kwenye majani hususani sehemu za chini ya majani..
  6. Tumia dawa za kuua vidukari kama CONFIDOR, IMIDACLOPRID kwa kiwango kilichoelekezwa kwenye lebo.

Iwapo una swali lolote usisite kutuandikia kupitia info@mkulimalife.or.tz. Pia endelea kutufuatilia katika mitandao ya kijamii kwa habari zaidi kupitia Facebook, Instagram, Twitter na Linkedin  @mkulima_life na @farmco_ltd